Subscribe:

Ads 468x60px

Pages

Saturday, May 7, 2011

BANZA ATUA EXTRA BONGO


Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’;

Mwalimu wa Walimu aliyetua Extra Bongo

Na Rachel Mwilligwa

KAMA kuna mwanamuziki ambaye nitabaki siku zote kutetea kwa nguvu zote kwamba ni alama ya mabadiliko katika muziki huu wa sasa, atakuwa si mwingine ila ni Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’.

Unaweza ukawa unamjua Banza Stone, lakini napenda kukufahamisha ni msanii huyu ambaye aliifanya African Stars ‘Twanga Pepeta’ ishike kasi yake na kuleta mapinduzi makubwa ya muziki wa dansi.

Ni wakati ambapo muziki kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ulipokuwa unashika kasi kubwa na ya aina yake, pale Banza Stone alipofanikiwa kuwabadilisha Watanzania na kuupenda muziki wao, japo kulikuwa na kuiga kwa hapa na pale.

Naamini Luiza Mbutu na Jesca Charles wanaweza kuwa mashahidi. Naisema ile Twanga Pepeta, ambayo ilikuwa inapigana kufa na kupona ili itoke, huku wasanii wake tukikumbana nao Mnazi Mmoja, wakitembea kwa miguu kwenda na kurudi mazoezini.

Unaikumbuka ‘Angurumapo Simba’? Hiki ni kibao ambacho kilishika chati kubwa, huku Twanga Pepeta ikiwa na wanamuziki wakali wakiwa chini ya uongozi wa Adolph Mbinga.

Mbinga ndiye aliyeibuka pia na nyimbo zilizopendwa pia na wengi kama ‘Kisa cha Mpemba’ na ‘Bwana Kijiko’. Banza ndiye aliyesimama kuimba nyimbo hizi na ghani zake za ‘kukohoa’.

Wakati yuko Twanga Pepeta, Ally Choki naye alikuwepo lakini tuseme wazi alikuwa hapewi nafasi kubwa. Banza ndiye aliyebaki kuwa alama ya bendi na aliweza kuipeleka mbele.

Alipoondoka wote walijua mwisho wa Twanga Pepeta umewadia, lakini hapo ndipo Choki naye alipoibuka juu na kuliziba vema pengo la Banza na safari ya bendi hiyo ikazidi kusonga mbele.

Choki naye akaja kuondoka na bado tukiri udhaifu ukaanza kuonekana na uongozi wa bendi hiyo ukalazimika kumrejesha kundini Banza Stone ‘Mwalimu wa Walimu’ akaja kuibuka na kitu kilichokwenda ‘shule’ zaidi.

Banza alikuja na kibao cha ‘Mtu Pesa’ ambacho ilifikia wakati hata uongozi wa bendi hiyo ulikiri kwamba albamu hiyo ndiyo ilikuwa bora zaidi kupata kutolewa na iliingizia fedha nyingi. Hawakutaka kutoa takwimu.

Hii achana na nyimbo nyingine nyingi alizotunga wakati akiwa TOT Band na toka aondoke katika kundi hilo, bendi hiyo imeshindwa kusimama.

Kumbukam Banza Stone alikuwa na vibao vingi tu hivi vikiwa baadhi kama ‘Aungurumapo Simba’, ‘Mtaji wa Maskini’, ‘Elimu ya Mjinga’, ‘Euro 2000’, ‘Mtu Pesa’, ‘Hujafa Hujasifiwa’ na ‘Mimi Niseme’.

Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, hatimaye Banza Stone ameamua kuungana na Choki katika bendi ya Extra Bongo ‘Next Level’ ili waanze kufanya kazi pamoja.

Mkurugenzi wa Extra Bongo, Ali Choki, alisema kuwa, amemchukua Banza Stone ili kuongeza nguvu kwenye bendi hiyo ili iweze kuhimili ushindani wa soko uliopo sasa.

Kwa upande wake Banza Stone, alisema amesaini mkataba wa mwaka mmoja kuifanyia kazi Extra Bongo akiwa na lengo la kuongeza nguvu zaidi na ni njia mojawapo ya kutodumaza kipaji chake.

Banza Stone atatambulishwa rasmi Mei 26, katika onyesho maalumu ingawa kwa sasa ataendelea kufanya kazi na bendi hiyo hadi siku ya utambulisho itakapofika.

Mashabiki kwa sasa watataka kuona kama watu hao wawili wenye historia kubwa ya muziki, kama watafanikiwa kutoa kitu kikali zaidi ambacho kitapendwa na mashabiki wao.

Choki alitamba kwa sasa ana uhakika bendi yake itafika mbali, kwani ina kila kitu cha kujivunia ikiwa pamoja na kuwepo kwa wasanii wakali zaidi na wanaojua nini wanachofanya wanapokuwa jukwaani.

“Kwa sasa tuna kila kitu cha kujivunia, kwani bendi yetu imeanza kupata wakali wa kuwategemea na naamini kabisa baada ya muda mchache watatutambua sisi ni nani,” alisema msanii huyo.

Banza alidai kwa sasa yeye ni vitendo tu na watu wakae mkao wa kula kwa kuona vitu vikali zaidi, ambavyo anaamini wengi watavihusudu na hasa kufanya kazi kwa pamoja na Choki.

Nini kitakachotukia? Ni wakati wa kusubiri tu na kuona ambacho mafahari hawa wawili watakifanya.


0 maoni:

Post a Comment