BENDI ya Extra Bongo 'Wazee wa Kizigo', inatarajia ziara ya
utambulisho wa albamu ya 'Mtenda Akitendewa' kwenye mikoa ya Kanda ya
Kusini ya Lindi na Mtwara.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa bendi hiyo Ally Choki, utambulisho huo
utakwenda sambamba na wa mwimbaji mpya Khadija Mnoga 'Kimobitel'
aliyejiunga na Extra Bongo hivi karibuni.
Choki aliliambia gazeti la NIPASHE kuwa ziara hiyo itaanza leo
Jumatano ambapo itafanya utambulisho wa kwanza Kilwa mkoani Lindi
katika ukumbi wa Jumba la Dhahabu.
Mkurugenzi huyo alisema kuwa kesho bendi hiyo itakuwa mjini Ruangwa
mkoani Lindi ikiendelea na utambulisho huo katika ukumbi wa Yongolo na
kisha Ijumaa ndani ya ukumbi wa MB Pub mjini Masasi mkoani Mtwara.
"Baada utambulisho huo wa mjini Masasi tutaelekea Lindi mjini na
kumalizia ziara ya utambulisho wa albamu na Kimobitel ndani ya ukumbi
wa Bwalo la Maofisa wa Polisi," alisema Choki.
Alifafanua kuwa baada ya utambulisho huo Extra Bongo itarudi jijini
Dar es Salaam kujipanga kwa ajili ya ziara nyingine ya mikoa ya Kanda
ya Ziwa Victioria ikiwemo ya Mara, Mwanza na Gaita.
"Tukimaliza ziara ya Kanda ya Ziwa na tutarudi Dar es Salaam kuandaa
sherehe ya bendi yetu kutimiza miaka mitatu tangu ifufuliwe upya
ambapo pia tutaingiza sokoni albamu yetu," alisema.